Miili ya watu wapatao 129 imepatikana kutoka Ziwa Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, baada ya feri kupinduka na kuzama mapema Ijumaa.
Waziri wa Uchukuzi nchini humo Laurent Sumba Kahozi amesema
msako unaendelea kuwatafuta watu waliopotea katika ajali hiyo.
Wafanyakazi wa uokoaji waliwapata abiria wakielea katika maji
Jumapili, wakiwa katika mapipa ya petroli na vifaa vingine.
Habari zinasema ajali kama hiyo ni za kawaida katika eneo hilo
kutokana na boti kujaa abiria na mzigo kupita kiasi.
Maboya ya kujiokoa mara nyingi hayamo katika maboti hayo na watu
wengi hawawezi kuogelea.
Maafisa katika jimbo la Katanga wamesema upepo mkali na kujaza abiria na
mizigo kupita kiasi kumesababisha boti MV Mutambala, kupinduka
Wanawake na watoto ni miongoni mwa watu waliokumbwa na ajali
hiyo ambayo ilitokea mapema Ijumaa asubuhi.
Taarifa za awali zilisema watu 26 wamekufa katika ajali hiyo.
Idadi ya watu walionusurika imetajwa kuwa watu 232, wengi wakiwa
ni wanaume, amesema waziri wa uchukuzi katika eneo hilo.